
Huenda akizungumza unaweza usimwelewe, lakini Diamond Platnumz
aliamua kufikiri nje ya boksi na kufanikiwa kufanya kile alichokuwa
akikikusudia, leo hii tayari makumi ya wasanii wameanza kutembea katika
nyayo zake.
Kwa mujibu wa staa huyu ambaye alifanya mahojiano
ya ana kwa ana nyumbani kwake Sinza jijini Dar es Salaam, anasema
lilikuwa ni wazo lake tangu mwaka 2009 alipoingia rasmi katika muziki
kwa kuweka nadhiri kwamba lazima ahakikishe anaitangaza nchi yake
kupitia sanaa.
Anasema ilikuwa safari ndefu yenye milima na
mabonde, lakini amefanikiwa kufikia hatua za mwanzo na anaamini bidii
ikiongezwa kwake na wasanii wengine, muziki huo utafika mbali.
“Muziki wa Tanzania kwa sasa unaenda kasi mno,
ukiangalia msanii Shetta wimbo wake wa ‘Kerewa’ unapigwa karibu redio za
Fm sita hivi tunavyoongea wiki hii, wimbo wake umeshika nafasi ya tatu
kwenye Beat Fm ya jijini Lagos, zamani kibongobongo suala kama hili
lilikuwa ndoto na halikuwezekana kabisa.”
Diamond anasema mitandao ya kijamii imechangia kukua kwa soko lao, lakini jitihada binafsi za wao wenyewe zimesaidia.
“Ukiangalia katika vyombo vya habari hasa mitandao
namna watu wanavyojitangaza, video zinavyofanyika ni tofauti na zamani.
Tulikuwa tunafanya muziki lakini tulikuwa hatujitangazi, sasa hivi
msanii akitoa singo anatengeneza kava, matangazo, watu wanafanya muziki
kama biashara, wanapanda jukwaani na madansa yaani nidhamu ipo katika
muziki tofauti na zamani,”.
Hata hivyo, Diamond anasema anakumbana na
changamoto nyingi hivi sasa katika maandalizi ya kazi zake kwani ana
soko kubwa la ndani lakini
pia
soko pana la nje ambako analazimika kuwalisha mashabiki wake wapya.
“Mwenyezi Mungu kanijalia kuna mashabiki
wananikubali na wananiamini ndani na nje ya nchi, changamoto ninayoipata
kwa sasa ni kuhusu mashairi ya kazi zangu, nitatengeneza vipi wimbo
ambao nje utaeleweka?” anahoji na kuongeza:
“Soko la Tanzania linachanganya, watu wanataka
niimbe mtu kaachwa lakini mwenyewe naangalia hivi wimbo kama huu nje
utakubalika? Yaani hicho ndiyo kitu kinachokuwa kinanivuruga akili yangu
kwa hiyo inabidi huku nifanye wimbo wake na nje wake ndiyo maana hata
ukiangalia katika wimbo wa ‘Bum Bum’ na ‘Mdogo Mdogo’ kuna vionjo
tofauti,” anasema.
Licha ya ugumu wa kazi aliyonayo, anasema bado
mapromota wamekuwa wagumu kuelewa na kurekebisha malipo ya wasanii,
tatizo linalosababisha wengi kukata tamaa.
“Ningependa tukimbizane katika soko la kimataifa,
lakini tatizo wasanii walio wengi na wenye uwezo wanalipwa malipo
kiduchu yasiyolingana na kazi zao, wataweza vipi kufanya kazi zenye
viwango kama ninavyofanya mimi?”
“Tatizo lipo kwa hawa mapromota, mtu hataki
kukubali kwamba kuna kitu kimebadilika, kukubali kwamba wasanii nao wapo
katika soko na inatakiwa muziki ubadilike, mapromota wakubali kwamba
tunataka haya yarekebishwe ili muziki ubadilike malipo ya shoo yapande
wasanii bado wananyonywa, lakini mimi sikubali hata siku moja ndiyo
maana nimejitengenezea jina langu kwenye biashara,” anasema Diamond.
No comments:
Post a Comment