

REHEMA Chalamila ndilo jina lake ingawa mashabiki wengi wa muziki wa kizazi kipya wanamfahamu kama Ray C. Bongo Fleva itakuwa haimtendei haki, kama historia haitamtaja kama mmoja wa wasanii waliotoa mchango mkubwa kwenye aina hii ya muziki ambao sasa, unatamba barani Afrika.
Ni miongoni mwa mabinti wa kwanza kwanza kuingia katika ‘game’ na uwezo wake mkubwa katika kucheza, hasa ile staili yake ya kuzungusha kiuno, ilimpatia mashabiki wengi, ndani na nje ya nchi kiasi kwamba wakati flani, alikuwa lulu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Ingawa hivi sasa hana makali kama enzi zile, lakini ni lazima kumpa pongezi kwamba angalau bado anaonekana katika fani, tofauti na wasichana wengine wa umri wake walioanza muziki ambao hivi sasa wamepotea kabisa.
Umaarufu wake hata hivyo, ulimzidi kiasi cha kujikuta akiwa mbwia unga, tabia ambayo kwa bahati mbaya imewakumba sana wasanii wengi wa muziki huu. Ni jambo la kushukuru kwamba aliweza kujitambua na kukiri jambo hilo hadharani, lililosababisha wadau, wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete kujitokeza na kumpatia huduma za kumuokoa na utumiaji wa madawa hayo ya kulevya!
Nina imani anaendelea vizuri na unywaji wa dawa za kumuweka sawa ili aachane kabisa na uteja, ingawa uzoefu unaonesha kuwa ni kazi kubwa sana kwa teja kuacha ‘kula sembe’.
Hivi majuzi Ray C alikuja na mpya. Kupitia akaunti yake katika mtandao wa Instagram, alitoa tangazo la kuhitaji mume wa kumuoa, akiorodhesha masharti kadhaa yanayopaswa kuzingatiwa na atakayemhitaji.
Anyway, ni masharti kama yalivyo hayana mjadala, licha ya kuwa yapo mengine muhimu zaidi ambayo kwa msichana wa hadhi yake alipaswa kuyaweka ili kuwaonesha watu jinsi gani alivyo siriaz na anachokisema!
Kwa mtu wa aina yake, aliyezurura sana enzi zake aking’aa, bila shaka wengi watatilia shaka kuhusu afya yake, hivyo lilikuwa ni jambo zuri kwake kuorodhesha zoezi la upimaji afya kama sharti la msingi ili kuwapa watu imani. Kama yale ndiyo masharti pekee, maana yake ni kuwa dada yupo tayari kuingia mzigoni na yeyote aliyekidhi vigezo alivyoweka, hata kama ana ngoma!
Kwa majaribu aliyopitia pia, lilikuwa jambo zuri kwake kumhitaji mwanaume mwenye hofu ya Mungu. Anajua kuwa kama siyo Muumba kusikiliza maombi yake, unga ungeendelea kumtesa. Lakini siyo suala la unga tu, katika maisha haya ambayo hatujui hatima yake, ni vyema kumchagua mwenza mwenye kuamini kikamilifu uwepo wa Mungu.
Na pengine baada ya kuwa na mume mwenye afya njema na mcha Mungu, hivi ni kweli Ray C hahitaji mtu mwenye kujituma ili kuyafanya maisha yaende? Nadhani anatakiwa kumpata mwanaume mwenye uwezo wa kutafuta hela kihalali, jambo ambalo hajaliorodhesha katika masharti yake.
Orodha ya mahitaji muhimu ya Ray C katika ndoa yake yanaonesha kama tayari anao wanaume mbele yake, wenye kujiweza ambao muda wote watawaza mapenzi tu. Kwa mfano, anaposema anahitaji mtu atakayetumia naye simu moja, kila sehemu wawe wote, hivi kwa maisha haya, mwanaume unapata wapi muda wa kuwa na mkeo muda wote kila mahali?
Hata hivyo, pengine nimwambie dada yangu Ray C kuwa katika maisha hakuna kuchelewa, ingawa kiukweli, hivi sasa angestahili kuwa tayari kwenye ndoa. Na labda yeye awe kama fundisho kwa wadogo zake wanaofanya muziki.
Wajaribu kufahamu kuwa ujana unaotumika katika starehe, ndiyo unaopaswa kuwa wakati wa kutengeneza kesho yao, vinginevyo nao wataishia kuhitaji ndoa kwa matangazo na kuwapa watu la kusema kama wanavyofanya sasa kwa Ray C.
No comments:
Post a Comment