
Mcheza filamu Shamsa Ford amesema kuwa alitunga filamu ya
Chausiku kuonyesha uwezo walionao baada ya kunangwa kuwa ‘anauza sura’
katika tasnia hiyo.
Ford alisema mara nyingi kumekuwa na maneno kuwa
waigizaji wasiopitia katika vikundi kama cha Kaole Sanaa Group, kazi yao
ni kutafuta umaarufu, shutuma za karibuni zikiwa zimetolewa na Nuru
Nasoro, maarufu kwa jina la Nora, ambaye aliwaelezea waigizaji
wanaochipukia kuwa ni “wauza sura” na hawana jipya.
Lakini Ford alisema kauli hiyo na nyingine nyingi
za kuwabeza, zilimuhamasisha kufanya kitu ili kuonyesha kuwa wanachotaka
kufanya kazi ndiyo maana akaibuka na filamu hiyo.
Alisema kwa kawaida yeye ni mpole sana, lakini katika filamu hiyo ameigiza mcharuko na asiyekwenda na wakati.
“Nakumbuka nilikuwa nimepumzika ufukweni nikiawaza
ni kwa jinsi gani nitaweza kuonyesha uwezo wangu binafsi. Kuigiza,
naigiza sana tu, lakini bado kazi yangu haionekani, badala yake
naonekana muuza sura,” alisema Ford.
Akizungumzia filamu hiyo ambayo ni gumzo hivi sasa, Ford alisema ametunga mwenyewe na inasimamiwa na kampuni ya Jerusalem Film.
“Hata sisi tunaweza na vipaji tulizaliwa navyo,
lakini wakati haukuruhusu kujikita kwenye mambo hayo na tulipopata
nafasi tumeweza kuonyesha jinsi gani tunaweza na bado wasubiri kutuona
zaidi na zaidi; huu ni mwanzo, ”alisema Ford.
Ford alisema licha ya kuwa na tabia ya upole,
hakupata shida kuigiza katika nafasi ya mcharuko kwa kuwa lilikuwa ni
wazo lake na aliyelitekeleza ni yeye na kwamba kama isingekuwa hivyo,
ingemchukua muda kidogo kuelewa mtunzi alikuwa anataka nini, kwa kuwa
siyo kitu cha kufikiria harakaharaka.
No comments:
Post a Comment