airport jogging

mavazi

aus521

aus9

Wednesday, April 15, 2015

JIDE KWENYE HILI LA MAZISHI YAKO MI’ SIKUELEWI!


SIKU zote amekuwa mfano bora kabisa wa msichana aliyeamini kubadili maisha kupitia kipaji na kujituma kwake, kwani wakati wasichana wengi wa kizazi chake katika muziki wa Bongo Fleva wakibakia kuwa historia, Judith Mbibo, tunayemfahamu sana kama Lady Jaydee, ameendelea kuwa juu kisanaa na bila shaka, kimaisha.
Tutakuwa tunapoteza nafasi kama tutaanza kujadili kazi gani alizofanya, zipi zilimpatia jina na nini alichokipata kupitia sanaa, lakini itatosha sana tukimtambua kama mmoja kati ya wasanii waliofanikiwa kulinda hadhi yake kimuziki kwa muda wote tangu alipoibuka pia kuonyesha kuwa muziki ni kazi kama zilivyo nyingine, tofauti na imani ya wazazi wengi kuwa sanaa hiyo ni uhuni.
Hii siyo mara yangu ya kwanza kuandika hapa kuhusu Jide na sidhani kama itakuwa ya mwisho. Siyo kwa sababu nina usongo naye, bali kwa vile yeye kama staa, ana nafasi kubwa ya kunivutia kumjadili tena, wakati huu akielekea katika miaka yake 15 katika muziki, akiendelea kubakia kileleni kwa ubora wa kazi zake na pia kama mfano mzuri wa mjasiriamali.
Wiki moja na ushee iliyopita, moja ya magazeti ya Global Publishers, yaliandika habari juu ya Lady Jaydee kutoa sampo ya jeneza lake, ambalo angependa azikwe nalo siku yake ikifika. Haishangazi, kwa sababu utamaduni huu umekuwepo kwa miaka mingi kwa mababu na mabibi zetu kujiwekea majeneza waliyopenda kuzikwa nayo.
Lakini kwa Jide, alisogea mbele zaidi kidogo alipodai katika mazishi yake, angependa wawepo watu walioalikwa tu, badala ya kila mtu kutaka kushiriki shughuli hiyo.Kimsingi, hiyo ni haki yake kabisa. Kila mtu anao uwezo wa kuamua lolote linalomhusu, ili mradi tu, havunji sheria zilizopo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wapi azikwe, azikwe kaburi la aina gani, nani aje nani asije ni matakwa ya mhusika na yatatimizwa. Kuna kitu kinaitwa Wosia, ukiandikwa, haukiukwi.
Tunao mfano wa wakili mmoja maarufu jijini Arusha, Nyaga Mawalla aliyejirusha ghorofani na kufariki kule Nairobi nchini Kenya. Katika wosia wake aliandika, endapo atafia nchini Tanzania, basi mwili wake uzikwe katika shamba lake lililopo Arusha, lakini endapo atafia nje ya nchi, azikwe hukohuko atakakofia.
Wengi mtakumbuka jinsi ilivyotokea tafrani kwa wazazi wake, ambao mwishowe walilazimika kukubaliana na kilichoandikwa na kijana wao!Lakini hata hivyo, upo umuhimu wa kuangalia aina ya wosia tunaoacha nyuma ya mauti yetu, kwa kuzingatia mila, desturi na tamaduni zetu kama wabantu. Jide anasema angependa wawepo waalikwa tu, sawa. Je, mauti yatakapomfika, tayari atakuwa amemteua mtu wa kutoa mialiko? Na labda, kuna majina au aina ya watu wanaostahili kualikwa?
Ninavyojua, mauti yetu ni fumbo kwa sababu hakuna ajuaje siku wala saa. Utamaduni wetu unaelekeza shughuli za mazishi kuwa ni za kila mtu. Ndiyo maana magari yanasimama barabarani kupisha watu waliobeba jeneza na baadhi yao, huweza kushuka na kusindikiza mwili.
Kwa mtu kama Jide, aliyetumia karibu nusu ya maisha yake kuishi mioyoni mwa watu kupitia muziki wake, sidhani kama alijishauri vizuri kabla ya kutoa kauli hiyo.Kuna watu wanatamani watoto wao waje kuwa kama yeye, wengine wako tayari kufanya kila wanachoweza kufanya angalau wapate nafasi ya kumshika mkono tu na roho zao zitatulia kabisa. Watu wa aina hiyo, wapo kila kona ya Afrika Mashariki na Kati ambako muziki wake unasikika.
Mtu kama huyo, kushindwa kushuhudia Jide akizikwa, huko Musoma au Dar es Salaam, kwa sababu tu hakuwa na mwaliko, ni ukatili. Kwa vile siyo utamaduni wetu, wengine wanaweza kuleta hata fujo mazishini kwa sababu hawataamini watakapoambiwa wanapaswa kuwa na kadi, maana mazishi sasa ni kama sherehe za harusi!

No comments:

Post a Comment