DAR ES SALAAM! Wakazi wa Mbagala
Chalambe jijini Dar es Salaam, waliamka asubuhi na kukutana na tukio
lililojaa maswali mengi huku majibu yakiwa haba kufuatia kukuta kitu
kaburini kikiwa kimeviringishiwa sanda.
ILIVYOKUWA
Kwa mujibu wa shuhuda wetu, tukio hilo
lilijiri hivi karibuni kwenye Makaburi ya Chalambe ambapo wakazi hao
walilizunguka kaburi hilo huku wakidai kuwa, ndani ya sanda hiyo
kulikuwa na mtoto aliyeuawa na kuwekwa hapo.
SHUHUDA ATOA
MAWAZO YAKE
“Jamani humu kwenye sanda kuna maiti ya
mtoto mdogo. Lazima kuna mahali ameuawa, wakamviringishia sanda maskini
wa Mungu, wakaja kumuweka hapa,” alisema mkazi mmoja akiwa amejikunyata
baada ya kutoka kulala.
MTAZAMO WA WENGINE
Wengine walisikika wakisema kuwa, kwa
vyovyote mtu au watu waliotupa kitu hicho walikuwa katika harakati za
ushirikina kutokana na maelekezo ya mganga.
“Huu ni ushirikina mkubwa, lazima watu
wamefanya hivi kwa maelekezo ya mganga. Huwezi kuja kutupa vitu vya
uchawi kwenye kaburi la mtu, watu hawana hata woga wala hawamuogopi
Mungu,” alisema mama mmoja.