DAR ES SALAAM! Wakazi wa Mbagala
Chalambe jijini Dar es Salaam, waliamka asubuhi na kukutana na tukio
lililojaa maswali mengi huku majibu yakiwa haba kufuatia kukuta kitu
kaburini kikiwa kimeviringishiwa sanda.
ILIVYOKUWA
Kwa mujibu wa shuhuda wetu, tukio hilo
lilijiri hivi karibuni kwenye Makaburi ya Chalambe ambapo wakazi hao
walilizunguka kaburi hilo huku wakidai kuwa, ndani ya sanda hiyo
kulikuwa na mtoto aliyeuawa na kuwekwa hapo.
SHUHUDA ATOA
MAWAZO YAKE
“Jamani humu kwenye sanda kuna maiti ya
mtoto mdogo. Lazima kuna mahali ameuawa, wakamviringishia sanda maskini
wa Mungu, wakaja kumuweka hapa,” alisema mkazi mmoja akiwa amejikunyata
baada ya kutoka kulala.
Wengine walisikika wakisema kuwa, kwa
vyovyote mtu au watu waliotupa kitu hicho walikuwa katika harakati za
ushirikina kutokana na maelekezo ya mganga.
“Huu ni ushirikina mkubwa, lazima watu
wamefanya hivi kwa maelekezo ya mganga. Huwezi kuja kutupa vitu vya
uchawi kwenye kaburi la mtu, watu hawana hata woga wala hawamuogopi
Mungu,” alisema mama mmoja.
POLISI WAITWA
Ili kutatua kitendawili hicho cha nini
kilikuwa ndani ya sanda, baadhi ya wananchi walikwenda Kituo cha Polisi
Mbagala Chalambe na kuripoti tukio hilo ambapo baadhi ya askari
waliongozana na watoa taarifa hao mpaka eneo la tukio.
Baada ya polisi kufika, macho ya kila
mtu yalikuwa na shauku ya kutaka kuona ndani ya sanda ile mlifungwa nini
ili waanze kutoa mitazamo yao.
KILICHOKUTWA
Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya
kawaida, baada ya polisi kuifungua sanda hiyo, kilichokutwa ndani ni
jogoo wawili ambao walikuwa hawana vichwa!
Watu walitawanyika, wengine
wakisikitika, wengine wakicheka lakini wapo pia waliokuwa wakilaani
tendo lile hasa kwa kuzingatia kuwa, lilifanywa juu ya kaburi la
marehemu ambaye ana ndugu zake walio hai hivyo kuzidisha majonzi kwao.
MZEE ALAANI
Mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la
Ally Mwanaisi akizungumzia tukio hilo, alisema dunia ndiyo imefikia
hapo, kwamba watu hawaogopi kufanya lolote.
“Hii ni dunia ya mwisho. Mtu anakuja
kufanya ushirikina wake kwenye kaburi la mwenzake bila woga. Hivi hao
waganga ndiyo wanawaambia kwa kufanya hivi mambo yao yatakuwa mazuri
siyo?” alihoji mzee huyo.
No comments:
Post a Comment